Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba umeingia katika sura mpya ambapo uteuzi wa wajumbe 201 wa Bunge la Katiba umekamilika.
Uteuzi huo unatawaliwa na Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, Sura, 83 ambayo inaweka mamlaka ya uteuzi, masharti, taratibu,
vigezo na mambo mengine yote yanayopaswa kuzingatiwa katika uteuzi wa
wajumbe wa Bunge la Katiba.
Sheria hiyo inataja aina tatu za wajumbe wa Bunge
la Katiba kuwa ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na wajumbe 201 kwa mujibu wa
Kifungu Na. 22(1c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inaonyesha
makundi mbalimbali 10 yanayohusika.
Makundi hayo ni pamoja na taasisi zisizokuwa za
kiserikali (20), taasisi za kidini (20), vyama vyote vya siasa vyenye
usajili wa kudumu (42) na taasisi za elimu (20).
Pia sheria inataka wateuliwe watu wenye ulemavu
(20), vyama vya wafanyakazi (19, vyama vinavyowakilisha wafugaji (10),
vyama vinavyowakilisha wavuvi (10), vyama vya wakulima (20) na vikundi
vya watu wenye malengo yanayofanana (20).
Kutokana na sheria na muundo wa Bunge la Katiba,
Chama Cha Mapinduzi (CCM) chenye wabunge wapatao 260 katika Bunge la
Jamhuri ya Muungano, kimeongezewa tena kwenye makundi yaliyotajwa hapo
juu, huku taasisi nyingine ambazo zilituma majina yake hata
hazikufikiriwa.
Ni kweli kwamba kulikuwa na majina zaidi ya 5,000
yaliyotumwa kwenye Ofisi ya Rais. Lakini kulikuwa na sababu gani ya
kuilimbikizia CCM majina zaidi wakati tayari ina wabunge wengi, na
kuyaacha makundi mengine yasiyo na harufu hata ya bungeni?
Kulikuwa na ulazima gani wa rais kuteua wajumbe?
Kama nafasi zilikuwa 201, kwa nini taasisi zisingeambiwa mapema zilete
wajumbe kulingana na nafasi hiyo? Labda kazi ya rais ingekuwa ni
kuthibitisha tu majina, lakini siyo kuwateulia watu wajumbe wasiowajua
kabisa.
Chukua mfano wa taasisi zisizokuwa za kiserikali
zenye wajumbe 20. Ukiiangalia orodha ile kwa hesabu ya haraka utaona
kuna makada waaminifu wa CCM watano na hilo ni kundi moja tu. Walau kila
kundi kuna makada watiifu wa CCM.
Kwa jumla CCM watakuwa na zaidi ya asilimia 70 ya
wajumbe wa Bunge la Katiba. Je, makundi ya watu wasio na sauti
yatasikilizwa? Hiyo Katiba itakuwa ya wananchi au ya chama tawala?
Sijagusia vyama vya siasa ambavyo walau vimekumbukwa kwa kupewa wajumbe wawili watatu. Lakini hawatafua dafu mbele ya CCM.
Kumbuka kuwa, CCM haikuwa na hata wazo la kuandika Katiba. Walidaka tu hoja za vyama vya upinzani na wanaharakati.
Hivi sasa ndiyo wamekamata usukani. Kama hawataki serikali tatu, basi wameshinda, kama wanataka kusimika utawala wao milele, hakuna wa kuwazuia. Kidumu Chama cha Mapinduzi.
Na Elias Msuya,Mwananchi
Hivi sasa ndiyo wamekamata usukani. Kama hawataki serikali tatu, basi wameshinda, kama wanataka kusimika utawala wao milele, hakuna wa kuwazuia. Kidumu Chama cha Mapinduzi.
Na Elias Msuya,Mwananchi
0 comments:
Post a Comment