Ni
muda wa wiki tatu sasa, dunia imepata mzizimo na simanzi kutokana na
kifo cha mtoto wa Afrika, shujaa, mpenda haki na usawa na kipenzi cha
dunia, mtoto huyo ni Nelson Mandela. “Madiba.”
Mandela hayupo duniani, na kamwe hatutamuona tena katika umbile lake
halisi la kibinadamu wala kusikia sauti yake hai na tamu inayorindima na
dhana za huba, busara na nasaha. Achilia mbali msimamo wake wa kusamehe
waliomkosea.
Madiba
ametangulia mbele ya haki. Wala hakufanya kosa. Hata mimi na wewe
tutakwenda huko. Ni lazima. Kumbuka hata wazazi wake walikwisha
mtangulia; na leo, yeye amewafuata, lakini hatawaona. Ni mapenzi ya
Mungu.
Wewe
na mimi tungependa tuendelee kuwa naye. Afrika na dunia ingependa
kuendelea kumlea, kumtunza na kumliwaza, lakini Mwenyezi Mungu amempenda
zaidi yetu. Amemchukua.
“Baba wa milele, mpokee katika makao yako ya milele mtumishi wako
uliomwita kutoka kwetu, Baba wa Afrika na kipenzi cha umma.” Amin!
Kusema
ukweli nilijipurukusha kutoandika neno lolote kuhusu kiongozi wangu,
masha’allah Nelson Mandela kwa sababu watu wengi wameandika habari zake.
Lakini purukushani zangu hazikufua dafu. Imenibidi kushika kalamu na
kuandika.
Dunia
ni ukumbi mpana wenye kila tendo la raha na karaha. Wenye vitamu na
vichungu. Uliojaa mapenzi na maovu, furaha na huzuni. Yote hayo Mandela
ima ameyaona, ameyasikia au ameyatenda. Hatimaye ameyapa kisogo na dunia
bado yamuhitaji.
Tangu
Desemba 5, 2013 mara tu taarifa ya kifo chake kutangazwa, hadi leo,
waandishi kadha wa kadhaa wameandika na kusimulia kuhusu nasaba,
makuzi, tabia, sifa, hadhi na uadilifu enzi za uhai wake.
Jumapili,
Desemba 15, 2013 Nelson Mandela amezikwa kijijini kwake Qunu katika
Jimbo la Cape Mashariki kwenye makazi yake ya milele. Maombolezo
yataendelea na maadhimisho ya kumbukumbu zake yatafanywa na kizazi cha
leo na vijavyo.
Si
nia yangu kukujaza maumivu na majonzi makali kuhusu hayati, isipokuwa
nimetingwa na hoja nzito na kujiuliza, Mandela ataenziwa au atakumbukwa
na watu waliomfahamu, waliofanya kazi naye au waliomsikia?
Nauliza
hivyo kwa sababu baadhi ya viongozi, watendaji na watumishi duniani na
hasa Afrika, wameonekana na kusikika wakilia kwa uchungu, na kumjaza
sifa njema kemkem na kusema, “tuyaenzi mambo yake mema.”
Viongozi hao wametukumbusha na kutusisitiza, kujifunza kutoka kwa Mandela tabia ya kusamehe. Kutenda haki na kujali usawa.
Mandela
si kiongozi mwadilifu wa kwanza wa Afrika kufariki dunia. Wapo wengi
waliomtangulia katika kundi lao la kupigania uhuru, haki, umoja na
usawa. Wao ni viongozi wakombozi wa mwafrika wa leo.
Baadhi
yao ni Kwame Nkrumah wa Ghana, Modibo Keita wa Mali, Gamal Abdel Nasser
wa Misri, Sir Abubakar Tafawa Balewa wa Nigeria na Julius Kambarage
Nyerere wa Tanzania. Wote hao wametufunza suala la uzalendo na ukombozi
wa Mwafrika.
Je,
viongozi wetu wa Afrika ya leo, wanaenzi kauli na matendo hayo yenye
busara, uzalendo, haki na usawa? Au wanakumbuka visa na vitimbi vya
baadhi ya viongozi wachache vya kufanya maovu, mauaji, na kuwa matajiri
na kuishi kifahari?
Kumbukumbu
bado zinatuonesha Afrika na watoto wa Afrika bado maskini. Lau kama
juhudi zilifanywa na viongozi tangulizi za kupata uhuru kututoa utumwani
na kutukomboa kifikra na kiuchumi. Afrika bado inahujumiwa.
Wakati
tunaendelea kuomboleza kifo cha Nelson Mandela, naunga mkono kauli ya
aliyekuwa Katibu Mtendaji wa tatu wa Kamati ya Ukombozi wa Bara la
Afrika, Brigedia Jenerali Hashim Mbita, alipozungumza na JAMHURI wiki iliyopita.
Nanukuu,
“Mandela ni aina ya viongozi ambao Afrika ilikuwa inawazalisha zamani.
Naweza tu kusema kwamba joto lile la kunyonywa, kubaguliwa na utumwa
ndilo lililozalisha viongozi waliokuwapo wakati huo. Sasa hivi
wamekuwa adimu kwa sababu joto lile lililowapika akina Mandela, Nyerere,
Kaunda na wengine halipo tena.
“Tusijaribu kulinganisha viongozi wa zamani na wa sasa. Mazingira ni
tofauti. Joto lililopo sasa hivi la utandawazi, teknolojia uzalendo na
umajumui wa Afrika ndilo hilo hilo linalotakiwa kuwapika viongozi wetu
wa kizazi kijacho” mwisho wakunukuu.
Maelezo
hayo kwa mtazamo wangu yanakumbusha viongozi wetu wa leo kuandaa
viongozi wajao katika mazingira yaliyopo kama walivyoandaliwa wenzao.
Pili waoneshe uzalendo wao katika harakati za kulinda, kugawa na kutumia
rasilimali za Afrika kwa haki na usawa.
Wazalendo wa Afrika tuko tayari kusamehe. Je, viongozi wetu wako tayari kuacha mali? Huko ndiyo kusamehe
Imeandikwa na Angalieni Mpendu, Dar es Salaam
Imeandikwa na Angalieni Mpendu, Dar es Salaam
0 comments:
Post a Comment