Jonas Mkude akisaini rasmi mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Simba huku Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspoppe (kushoto) na Rais wa klabu hiyo, Evance Aveva (kulia) wakishuhudia jana |
Wakati uongozi wa klabu ya soka ya Simba jana ukifanikiwa kumsainisha
mkataba mpya wa miaka miwili kiungo wake tegemeo, Jonas Mkude, sasa
klabu hiyo yenye Makao Makuu Mtaa wa Msimbazi Kariakoo jijini Dar es
Salaam inatarajia kupeleka maombi rasmi ya kumsajili mchezaji wa Yanga,
Simon Msuva.
Simba ilitangaza kumsajili Mkude bila ya kutaja dau, lakini habari zilizopatikana jijini zilieleza kuwa nyota huyo amesaini mkataba mpya baada ya kupewa kiasi cha Sh. milioni 60, gari aina ya GX 115 lenye thamani ya Sh. milioni 15 na mshahara wa Sh. milioni 1.2 kila mwezi.
Habari zaidi zinaeleza kwamba, Mkude, alikataa ofa ya Yanga ambayo ilikuwa imefika Sh. milioni 85 na kiasi ambacho hakijajulikana kutoka kwa Azam baada ya kuelezwa na mama yake kuwa anatakia aiheshimu Simba.
"Mama yake Mkude pia amechangia mtoto wake kubaki Simba, alimweleza asigombane na Simba kwa kiasi kidogo ambacho Yanga walitaka kumpatia," alisema rafiki wa karibu wa kiungo huyo ambaye kipaji chake kilianza kuonekana akiwa na timu ya vijana ya umri chini ya miaka 20 (Simba B).
Jana saa 6:40 mchana, Rais wa Simba, Evans Aveva, alimtambulisha Mkude mbele ya waandishi wa habari na kusema kwamba wameamua kumpa mkataba mpya ili aweze kuendelea kuichezea timu hiyo.
Aveva alisema maamuzi hayo yametokana na kuhitaji mchango wake ili kuifanya Simba iweze kupata matokeo mazuri uwanjani."Tumeshakamilisha kazi," alisema rais huyo ambaye aliingia madarakani Juni 29, mwaka huu.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspoppe, alisema kukamilisha zoezi la usajili huo kunamaanisha kuwa Yanga na Azam ambao walikuwa wanamuhitaji sasa wasijisumbue.
"Mkude ameamua kubaki Simba kwa sababu yeye hataki kucheza mchangani kama alivyoelezwa na (alitaja jina moja la kiongozi wa Yanga), yeye anataka kucheza uwanjani, na leo tumeamua kufanya wazi ili kila mmoja afahamu, mambo yetu ni hadharani," alisema Hanspoppe.
Mwenyekiti huyo wa usajili alisema kwamba wanapeleka maombi ya kumsajili Msuva kwa sababu wanaamini mchezaji huyo ni 'kijana' wao hivyo wanahitaji arejee nyumbani.
MKUDE- SIMBA IMENIKUZA
Saa 6:43, Mkude ambaye alishuka katika gari alilonunuliwa na klabu hiyo anasaini mkataba mpya wa kuichezea Simba kwa muda wa miaka miwili ijayo.
Alisema kuwa ameamua kusaini mkataba huo mpya baada ya kufikia makubaliano na viongozi wa Simba na ameahidi kuitumikia kwa juhudi timu hiyo iliyokuza kipaji chake.
Mkude alisema amefikia maamuzi hayo baada ya Simba kutekeleza makubaliano yote ambayo waliyafanya katika mazungumzo hivi karibuni.
"Maisha ni sehemu yoyote, lakini kwa sasa si wakati wake kuondoka Simba, wamenipa kila kitu nilichotaka, nitacheza kwa juhudi kwa sababu safari yangu bado haijatimia," alisema mchezaji huyo.
Aliongeza kuwa tabia yake haitabadilika na kuwataka mashabiki wa Simba wasubiri kuona 'makubwa' kutoka kwake
0 comments:
Post a Comment