Wizara
ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa taarifa ya
ugonjwa wa Figo ambapo katika tafiti mbalimbali zimezofanywa inaonyesha
kuwa ugonjwa huo upo na unaendelea kuongezeka nchini.
Kaulimbiu
ya Maadhimisho ya Siku ya Figo mwaka 2016 ni “Chukua Hatua Mapema
Kuepuka Magonjwa ya Figo kwa Watoto”. Kauli mbiu hii inalenga
kuhamasisha jamii juu ya matatizo ya figo yanayoikabili jamii yetu
hususani watoto.
Kwa
watu wazima chanzo kikubwa cha magonjwa ya figo ni ugonjwa wa kisukari
na shinikizo la damu, pia utumiaji wa dawa za mitishamba na magonjwa ya
kuambukiza kama ilivyo kwa watoto yanaweza kuathiri figo kwa watu
wazima, yapo pia magonjwa mengi ambayo huathiri figo moja kwa moja mfano
mawe ya figo na njia ya mkojo.
Tafiti
za ugonjwa wa figo zinaonyesha kuwa kati ya mwezi Agosti 2014 na
Februari 2015 kati ya watoto 513 waliopimwa magonjwa ya figo katika
Hospitali za Bugando na Sekou Toure asilimia 16.2% walikuwa na matatizo
ya figo. Katika utafiti huo ilionekana watoto waliokuwa na magonjwa ya
figo walikuwa na malaria, ugonjwa wa seli mundu (sickle cell anaemia)
maambukizi ya bakteria kwenye koo na ngozi na kutumia mitishamba kabla
ya kufika Hospitali. Utafiti huu unaonyesha wazi uwepo wa matatizo ya
figo kwa watoto.
Utafiti
mwingine uliofanyika Mkoani Kilimanjaro kati ya mwezi Januari na Juni
2014, uliohusisha watu 481 kutoka katika kaya 146, asilimia 7%
walionekana kuwa na matatizo ya figo. Utafiti huu ulionyesha uhusiano wa
karibu kati ya uwepo wa tatizo la figo na ugonjwa wa kisukari,
shinikizo la damu na matumizi ya mitishamba.
Serikali
inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya (2007) ambayo inalenga kutoa
huduma kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo matatizo ya figo.
Aidha, Serikali, Sekta Binafsi, Mashirika ya Kimataifa na Taasisi
zinazotoa huduma bila faida zinaendelea kuandaa na kurekebisha Sheria,
Kanuni na Taratibu zinazoimarisha uzuiaji na udhibiti wa magonjwa yasiyo
ya kuambukiza.
Hospitali
zenye wataalamu wa magonjwa ya figo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili,
Hospitali ya KCMC, Hospitali ya Rufaa Mbeya, Hospitali ya Bugando na
Hospitali ya Benjamin William Mkapa iliyopo Dodoma na mpaka sasa
wagonjwa 190 wakiwemo watoto wawili wamepata huduma ya kupandikizwa figo
na wanapata huduma katika kitengo cha figo Muhimbili na katika
Hospitali nyingine za rufaa.
Pia
Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha huduma za upandikizaji wa figo
zinapatikana hapa nchini haraka iwezekanavyo ili kupunguza gharama za
kupelekwa wagonjwa nje ya nchi na kutoa huduma kwa watanzania wengi
zaidi.
Aidha
Wizara inatoa wito kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anapima afya
yake na kwa wale ambao wameshajitambua kuwa na matatizo ya figo,
kisukari na shinikizo la damu lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo,
wanaaswa kutumia huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na
kuepusha athari zinazotokana na magonjwa hayo.
0 comments:
Post a Comment