Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), mkoa wa Singida, Diana Chilolo, amewashauri wakazi wote mkoani hapa bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, kuunga mkono kwa vitendo falsafa ya rais Dkt. Magufuli ya ‘HAPA KAZI TU’ kupitia matumizi ya simu za viganjani ili moto wa falsafa hiyo uwe endelevu.
Chilolo ametoa wito huo juzi wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa wadau wa elimu wa kata ya Ulemo wilaya ya Iramba ambapo alisema kuanzia sasa tujenge utamaduni kwamba kila mkazi wa mkoani hapa,akipigiwa simu na kusikia neno ‘haloo ajibu ‘HAPA NI KAZI TU’ alafu ndio aanze kumsikiliza mtu aliyempigia simu.
Alisema hiyo ndiyo njia pekee itakayokuwa chachu kwa wakazi wa Singida, kuchapa kazi kwa bidii.
 Alisema falsafa hiyo ya ‘HAPA NI KAZI TU’, lengo lake ni kuwatoa watanzania kwenye lindi la umaskini na kuwafikisha katika uchumi wa kati au zaidi.
“Ndugu zangu Rais wetu Dk.Magufuli ameanza vizuri kwa kupiga vita kwa nguvu zake zote uchumi wa  nchi ambao ulikuwa ukimilikiwa na watu wachache na kuurejesha kwa wananchi, kama kila Mtanzania atatekeleza kwa bidii na maarifa falsafa ya hapa ni kazi tu, nina uhakika nchi hii itafika wakati haitakuwa na omba omba” alifafanua.
Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo, ametumia fursa hiyo kumpongeza diwani (CCM) wa kata ya Ulemo, Samwel Shilla kwa ubunifu wake kuandaa mkutano wa wadau wa elimu kwenye kata yake.
“Elimu ni mwarobaini wa kila kitu, kwa mfano mkulima, mfugaji au mfanyabiashara mwenye elimu, shughuli zake zitakuwa ni zenye tija zaidi, kwahiyowa hiyo diwani umeona mbali, katika sekta ya elimu utaipaisha kata yako kimaendeleo,” alisema mwenyekiti huyo.
Na Nathaniel Limu, Iramba