WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema shule za sekondari za kata zina fursa ya kufanya vizuri kama
zilivyo shule nyingine licha ya kuwa watu wengi wamekuwa wakizidharau.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Jumatatu, Machi 7, 2016) wakati akikabidhi zawadi ya kompyuta mpakato
(laptop) kwa mwanafunzi aliyeshinda shindano la kuandika insha katika
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC ). Kompyuta hiyo ina
thamani ya sh. 1,992,000/-.
Mwanafunzi huyo, Jabir Mandando
(20), amehitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Mbekenyera
iliyoko wilayani Ruangwa mkoani Lindi. Amepata ufaulu wa daraja la pili
na sasa anasubiri matokeo ya kujiunga na kidato cha tano. Lakini
aliandika insha hiyo mwaka jana wakati akiwa kidato cha nne.
“Huyu ni mtoto wa kijijini tu.
Anatoka kijiji cha Namilema wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi. Shule ya
Mbekenyera aliyosoma ni shule ya kata. Ameweza kushinda tuzo na kushika
nafasi ya tatu katika shindano lililoshirikisha shule nyingi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki.”
“Jabir ameweza kuchomoza kitaifa kwa kushiriki shindano la kimataifa. Nimeamua kumpa zawadi ya laptop
pamoja na begi lake ili aweze kujisomea zaidi na kupata elimu ya
masuala mbalimbali kwa kutumia kompyuta hii. Pia nataka iwe ni chachu
kwa vijana wengine kushiriki mashindano kama haya,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu pia alikabidhi
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Shanael Nchimbi fedha taslimu sh.
500,000/- zikiwa ni zawadi kwa ajili ya shule hiyo. mwalimu Nchimbi
alimsindikiza mwanafunzi huyo Arusha kupokea zawadi hizo kwenye mkutano
wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliomalizika Arusha wiki
iliyopita.
Kwa upande wake, kijana Jabir
alisema anashukuru sana kwa zawadi aliyopewa na kuahidi kuwa atajitahidi
kusoma kwa bidii masomo ya kidato cha tano na sita ili aweze kutimiza
ndoto yake ya kuwa daktari.
Alipoulizwa alipataje taarifa ya
uwepo wa shindano hilo, Jabir alisema: “Walimu walipata taarifa
wakazileta darasani na kutuambia tushiriki kuandika. Walizikusanya na
kuchagua tatu bora, ndipo yangu ikashinda.”
Amesema insha aliyoiandika ilihusu: “The importance of political stability in the East African Integration.”
Alimwonyesha Waziri Mkuu cheti na
dola za Marekani 200 ambavyo alipewa zawadi kutokana na ushindi huo.
Shule ya Mbekenyera ambayo alikuwa akisoma, pia ilizawadiwa laptop na printer kutokana na ushindi wa kijana Jabir.
Mshindi wa kwanza katika shindano
hilo ametoka shule ya Sekondari Mzumbe, mshindi wa pili alitoka Kenya
na wa tatu alitoka shule ya Mbekenyera.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
- S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
JUMATATU, MACHI 7, 2016.
0 comments:
Post a Comment