Wabunge wa upinzani wamewasilisha kwa Spika wa Bunge hoja ya kumwondoa
madarakani Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kwa kutokuwa na imani naye.
Hatua hiyo imefikiwa na wabunge hao kufuatia kutoridhishwa na mwenendo wa uongozi wa Dk Tulia anapokalia kiti cha Spika.
Tangu Jumanne wiki hii, wabunge hao wamekuwa wakisusa vikao vinavyoongozwa na kiongozi huyo kwa madai anaminya demokrasia.
Walifikia
uamuzi huo baada ya Dk Tulia kuzuia kujadiliwa hoja ya kufukuzwa kwa
wanafunzi zaidi ya 7,000 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) iliyowasilishwa
na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na kukatisha mjadala wa
bajeti ya maji.
Kitendo hicho kiliwafanya wabunge wote wa upinzani kupingana na maamuzi ya Dk Tulia, jambo lililosababisha watolewe bungeni.
Kutokana
na hali hiyo wabunge hao kupitia Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya
akisindikizwa na Mbunge wa Kibamba, John Myika wa Chadema na Mbunge wa
Konde wa CUF, Khatibu Said Haji waliwasilisha hoja hiyo kwa Katibu wa
Bunge, Dk Thomas Kashilillah baada ya Spika, Job Ndugai kutokuwapo
bungeni.
Hoja hiyo iliwasilishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 138 (1) ambayo inaeleza utaratibu wa jinsi ya kumwondoa Naibu Spika.
Kanuni
hiyo inasema, “Utaratibu wa kumwondoa Naibu Spika madarakani chini ya
Ibara ya 85(4)(c) ya Katiba utakuwa kama ule wa kumwondoa Spika,
isipokuwa tu taarifa ya kusudio la kumwondoa Naibu Spika madarakani
inayoeleza sababu kamili za kuleta hoja hiyo, itapelekwa kwa Spika
ambaye ataiwasilisha kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
kwa ajili ya kuijadili.”
Fasili ya pili ya Kanuni hiyo inasema:
“Endapo Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itaridhika kuwa
zipo tuhuma mahususi dhidi ya Naibu Spika zinazohusu uvunjaji wa Katiba,
Sheria au Kanuni zinazoongoza Shughuli za Bunge, basi Kamati hiyo
itaidhinisha kuwa hoja hiyo ipelekwe bungeni ili iamuliwe.”
Kwa
mujibu wa Ibara ya 85(4)(c), Naibu Spika atakoma kuwa Naibu Spika na
ataacha kiti cha Naibu Spika endapo ataondolewa kwenye madaraka ya Naibu
Spika kwa azimio la Bunge.
Akizungumzia uwasilishwaji wa hoja hiyo, Millya alisema taarifa zaidi watatoa leo kuhusu msimamo wao huo.
Dk
Tulia aliwataka wabunge wenye malalamiko juu ya utaratibu wa uendeshaji
wa shughuli za Bunge kukata rufaa kwa kufuata Kanuni za Bunge.
Alisema
kanuni ndogo ya 5(2) inasema Spika atawajibika kutilia nguvu kanuni
zote za Bunge na 5(3) inasema Spika anaweza kumtaka mbunge yeyote
anayekiuka kanuni hizi kujirekebisha mara moja.
Alisema kwa hiyo mbunge yoyote asiyeridhika, kanuni za Bunge zinamruhusu kukata rufaa na zinamweleza nini cha kufanya.
0 comments:
Post a Comment