Roho Mtakatifuni Mungu, mwenye nguvu zote, maarifa yote,
anayepatikana kila mahali. Yeye pia anayo nafsi na kwa hiari yake
ameamua kuishi ndani ya mwili wa mwanadamu kwa kuzingatia mgawanyo wa
majukumu waliyokubaliana yaani nafsi ya Mungu Baba, Mungu Mwana(Yesu)
na Mungu Roho Mtakatifu. Kazi/lengo kubwa la ujio wake ni kuwa Msaidizi
wa mwanadamu kwenye ulimwengu huu wa mwili, ili kumsaidia kuishi katika
mapenzi ya Mungu.
Mungu hana namna ya kutawala kwenye ulimwengu wa kimwili bila kuwa
na mwili wa damu na nyama, kwa kuwa yeye ni Roho (Yohana 4:24). Hivyo
hana budi kuingia kwenye mwili wa mtu na kufanya makao yake hapo, ili
kutawala na kumuongoza mwanadamu katika mapenzi yake (Yohana14:18, 23,
1Wakorinto 3:16-17, 6:19). Kwa sababu hii ni muhimu sana kwetu kutunza
mahusiano yetu na Roho Mtakatifu ili tusimzimishe katika maisha yetu.
Paulo akizungumza na ndugu wa Thesalonike alisema ‘Msimzimishe Roho’
(1Wthesalonike 5:19). Paulo alitoa maonyo haya kwa kuwa alijua,
Kumzimisha Roho Mtakatifu, kuna athari mbaya sana kwenye maisha ya
mwamini katika kulitumikia kusudi la Mungu na hata maisha yake ya
kawaida hapa duniani. Swali la msingi ni, kwa namna gani mtu anaweza
kumzimisha Roho Mtakatifu? Ukisoma tafsiri za kiingereza, Biblia ya
toleo la GNB katika mstari huu inasema ‘Do not restrain the Holy Spirit’
na toleo la KJV linasema ‘Quench not the Spirit’ (1Th 5:19).
Tafsiri hizi mbili zinapanua zaidi tafsiri ya kumzimisha Roho, katika
dhana mbili zifuatazo; moja kumzimisha Roho ina maana ya kumzuia Roho
Mtakatifu asitawale na kuongoza maisha yako kwa kukataa msaada wake
maishani mwako. Pili, kumzimisha Roho Mtakatifu ina maana ya kuishi
katika mazingira ambayo yanamfanya Roho Mtakatifu ashindwe kukusaidia.
Mazingira ambayo Roho Mtakatifu anaweza kuzimishwa
Kutokumpa nafasi akusaidie
Kwa mujibu wa Matahayo 14:16, Roho Mtakatifu ameletwa kwetu kama
Msaidizi. Kwa tafsiri, Msaidizi ni yule atoaye msaada pale anapohitajika
na kupewa nafasi ya kufanya hivyo. Vivyo hivyo na Roho Mtakatifu kama
hujampa nafasi ya kukusaidia (ingawa yupo ndani yako), hawezi kufanya
hivyo na kwa hiyo taratibu utakuwa unamfungia/unamzuia kukusaidia
maishani mwako.
Kukosa upendo
Ukisoma kitabu cha 1Wakorinto sura ya 13 na 14, utagundua kwamba
suala la upendo limepewa msisitizo wa kipekee kwa mtu ambaye anataka
kuona utendaji wa kazi wa Roho Mtakatifu kwenye maisha yake na kwa ajili
ya wengine pia. Upendo kwa mtu aliyejazwa Roho Mtakatifu ni moja ya
vigezo muhimu sana kwa Roho Mtakatifu kusema/kujifunua na kufanya kazi
ndani yako. Hivyo kukosa upendo ni dalili ya kumzimisha Roho Mtakatifu
ndani yako. Ndiyo maana Paulo anasema hata kama angekuwa na unabii, na
kujua siri zote na maarifa yote, pia kuwa na imani timilifu kiasi cha
kuhamisha milima, kama hana upendo si kitu yeye, naam ni bure tena ni
ubatili (1Wakorinto 13:1-3).
Kuongozwa au kuenenda kwa mwili
Paulo aliwaambia hivi wandugu wa Galatia ‘Basi nasema, Enendeni kwa
kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili’ (Wagalatia 5:16).
Maneno haya alikuwa akiwaambia watu waliokoka na si wasiomjua Mungu.
Kanisa la Galatia lilikuwa limeacha kuenenda kwa Roho likaanza kuenenda
kwa mwili. Paulo akajua jambo hili litamzimisha Roho wa Bwana ndani yao,
na kwa sababu hii hawataweza kuishi maisha ya ushindi hapa duniani na
kisha kuurithi uzima wa milele, ndipo akawaonya akisema enendeni kwa
Roho ili msizitimize tama za mwili.
Kutokutii maelekezo yake
Roho Mtakatifu kuitwa Msaidizi haina maana tunapaswa kumpamngia cha
kufanya. Yeye ndiye mwenye kutuongoza katika njia itupasayo kuiendea
(Zaburi 32:8). Kinachotakiwa ni mtu kuwa mtiifu kwa yale ambayo Roho
Mtakatifu anakuagiza. Kukosa utiifu mara kwa mara kila
anapokusemesha/kukuagiza ni kumjengea mazingira ya kutoendelea kusema na
wewe na hivyo kuondoka kwako na kutafuta mtu mwingine amtumie kwa
kusudi lake.
Kukosa ufahamu wa utendaji wake
Mara nyingi watu wamemzimisha Roho kwa kutokujua utendaji wake
ulivyo. Kuna nyakati Roho Mtakatifu anaweza akaleta msukumo ndani ya mtu
wa kumtaka aombe, atulie kusoma neno n.k. Lakini kwa kutokujua namna
anavyosema, wengi hujikuta badala ya kutulia na kufanya kile alichopaswa
kufanya, wao hufanya mambo mengine.
Pia kuna nyakati katika ibada (sifa, maombi nk), Roho Mtakatifu
anaweza akashuka juu ya mtu au watu na akataka kusema jambo, lakini
viongozi wa makanisa au vikundi husika wakawazuia hao watu. Kufanya
hivyo bila uongozi wa Mungu ni kumzimisha Roho. Mandiko yako wazi kabisa
kwamba hatupaswi kutweza unabii (1 Wathesalonike 5:20) na wala
hatupaswi kuzuia watu kunena kwa lugha (1Wakorinto 14:39). Zaidi
tumeagizwa kujaribu mambo yote, na tulishike lililo jema (1
Wathesalonike 4:21).
Je tutajaribuje mambo yote ikiwa tunawazuia watu Kunena na pia
tunatweza unabii? Hofu yangu ni kwamba kwa kuzuia watu kunena na pia
kutweza unabii tunaweza tukajikuta tunamzimisha Roho Mtakatifu na
kukataa uongozi wake kwenye maisha yetu. Ni vema tukakumbuka kile
ambacho Paulo aliwaambia Wakorinto juu ya mambo haya kwamba ‘mambo yote
yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu’ (1 Wakorinto 14:40). Naam na hili
lina maana ni vema kwanza ujue utendaji wa Roho Mtakatifu ukoje, ili
kuepuka kumzimisha kwa kutokujua utendaji wake.
Pengine yapo mazingira mengine ambayo mtu anaweza akajikuta
anamzimisha Roho Mtakatifu. Kumbuka jambo hili kwamba kumzimisha Roho
Mtakatifu ni kumzuia asikusaidie, jambo ambalo tafsiri yake ni kukataa
uongozi wake kwenye maisha yako. Biblia inasema katika Warumi 8:9
‘Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili;
bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo
huyo si wake’. Usifanye mchezo na Roho Mungu hakikisha unatunza sana
mahusiano mazuri kati yako na yeye kwa kutokumzimisha.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nawe
Mwl Patric Sanga
0 comments:
Post a Comment