Habari Mpya

Saturday, May 04, 2013

Uhuru wa habari bado uko kitanzini




Leo tunaadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ambapo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), ikiwamo Tanzania husherehekea siku hiyo kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha wananchi na jumuiya ya kimataifa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari katika ustawi na maendeleo ya binadamu.
Baraza la Umoja wa Mataifa liliteua Mei 3 kila mwaka kuwa siku maalumu ya kutathmini na kuenzi kazi za waandishi wa habari na kuzikumbusha serikali duniani kote kuhusu wajibu wake wa kuheshimu, kutetea na kuunga mkono Uhuru wa Vyombo vya Habari kama inavyoelezwa katika Ibara ya 19 ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu.
Baraza hilo liliiagiza Unesco, ambalo ni shirika la UN linaloshughulikia masuala ya habari kuratibu shughuli za maadhimisho hayo katika kila nchi wanachama kwa kuwakutanisha waandishi wa habari, taasisi zinazojihusisha na uhuru wa waandishi wa habari na mashirika yaliyo chini ya UN ili kutathmini hali ya Uhuru wa Vyombo vya Habari katika nchi husika.
Hapa nchini mkutano wa kutathmini hali hiyo unafanyika jijini Arusha leo, ambapo Unesco inawakutanisha waandishi wa habari na taasisi zinazosimamia na kupigania uhuru wa vyombo vya habari. Mkutano huo unaoratibiwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa), Tawi la Tanzania utajadili masuala mbalimbali, huku msisitizo ukiwa juu ya usalama wa waandishi wa habari nchini kutokana na hivi karibuni baadhi yao kuuawa na wengine kushambuliwa, kutekwa na kutishiwa maisha, huku vyombo vya dola vikishindwa kuwakamata wahusika.
Hayo ndiyo mazingira ambayo mkutano wa leo jijini Arusha unafanyika. Ni mazingira ambayo tasnia ya habari inaonekana kuwa kitanzini, waandishi wa habari wakiwa wamejaa hofu ya kuuawa, kutekwa na kuteswa na maadui wa uhuru wa vyombo vya habari. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo juzi aliwashambulia waandishi wa habari mkoani humo kwa madai ya kuandika habari za kuwachafua viongozi wa Serikali, huku akionya hadharani kwamba kufanya hivyo wanaziweka roho zao rehani.
Kabla ya matukio hayo ya hivi karibuni, Tanzania ilikuwa moja ya nchi zinazolinda uhuru wa vyombo vya habari, licha ya Serikali kulifungia gazeti moja la kila wiki na redio mbili za madhehebu mawili ya dini. Rais Jakaya Kikwete binafsi amesimamia kukua kwa vyombo vya habari na ameonyesha uvumilivu mkubwa kila serikali yake inaposhambuliwa au yeye binafsi anapokosolewa. Tunaambiwa amekuwa akikataa shinikizo la washauri wake la kuvinyamazisha vyombo hivyo au kuwashushia rungu wahariri wake. Ndiyo maana matukio ya hivi karibuni dhidi ya wanahabari yamewashtua kwa namna ya pekee.
Wakati tukiutakia mafanikio mkutano huo wa wanahabari, tunategemea kwamba utatoa majibu ya matatizo yanayowasibu waandishi na tasnia yao ya habari hivi sasa. Pamoja na usalama wa waandishi, tunategemea tasnia hiyo ya habari ijitathmini, kwa maana ya kuchukua hatua za kulinda hadhi na maadili ya taaluma yenyewe.
Waandishi wengi hawajapewa mafunzo ya kutosha. Pamoja na kuzingirwa na mazingira hatarishi, wengi hawana bima ya maisha. Kwa hili waajiri wabanwe. Wakati huohuo, mkutano wa Arusha uhoji kwa nini Serikali haipeleki bungeni miswada ya Haki ya Kupata Habari na Huduma za Vyombo vya Habari.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Item Reviewed: Uhuru wa habari bado uko kitanzini Description: Rating: 5 Reviewed By: mcjohnminja.blogspot.com
Scroll to Top