Kichocho ni ugonjwa unaosababishwa na minyoo midogo aina ya Schistosoma
au Bilhazia ambayo huingia katika mwili wa binadamu kwa njia ya vitundu
vya ngozi na kusababisha mwasho katika viungo mbalimbali vya mwili na
kupelekea homa, mwili kudhoofu, kupungukiwa kinga mwilini na hatimaye
mtu kupoteza maisha.
Pamoja
na binadamu kuonekana kuugua ugonjwa wa kichocho pia wanyama wafugwao
kama vile Ng'ombe, Mbuzi na Kondoo hupatwa pia na ugonjwa huu wa
kichocho wanapotumia maji yaliyo na vijidudu vya maradhi hayo lakini
nitaelezea zaidi jinsi ugonjwa wa kichocho unavyoweza kumuathiri
binadamu.
Minyoo aina ya Schistosoma
ambayo hueneza Kichocho cha mkojo hasa kwa binadamu inatokea katika
Konokono waishio katika maji. Kichocho cha mkojo kwa binadamu husambazwa
na konokono wajulikanao kama Bulinus africanus, Bulinus tropicus na Bulinus forskalli, konokono hawa pia husambaza kichocho cha ng’ombe. Kichocho cha matumbo cha binadamu husambazwa na konokono waitwao Biomphalaria pfeiferi.
Minyoo
ikiwa katika hali ya lava inatoka kwenye Konokono na kuogelea katika
maji ikitafuta wanyama au binadamu wanaoingia kwenye maji hayo ili
waingie ndani yao kwa njia ya ngozi.
"Schistosoma
lava wakiwa katika maji hutoboa ngozi ya binadamu au mnyama aliyeingia
katika maji hayo na kuingia hadi kwenye mishipa ya damu mpaka kufika
kwenye maini ambapo hapo hubadilika na kuwa minyoo ambayo itaendelea
kukua na kuelekea katika sehemu mahsusi ya mwili ambapo minyoo wakubwa
hukaa " anasema Dkt. Jahashi Nzalawahe kutoka idara ya Vetenari
Microbaiolojia na Parasaitolojia ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
SUA.
"Kuna
aina kuu mbili za kichocho ambazo ni kichocho cha mkojo na kichocho cha
tumbo, Kichocho cha mkojo (Urinary schistosomiasis) husababishwa na
minyoo inayoitwa Schistosoma haematobium ambao huishi
katika mishipa ya damu ya kibofu cha mkojo cha binadamu na Kichocho cha
matumbo (Intestinal schistosomiasis) ambacho husababishwa na minyoo
iitwayo Schistosoma mansoni ambao hupatikana katika mishipa ya damu ya utumbo"
"Dalili
kuu za Kichocho cha mkojo ni kuwepo kwa damu katika mkojo, kujisikia
hali ya mwili kuchoka, kuwa na kikohozi kikavu na maumivu ya misuli, pia
dalili za Kichocho cha tumbo ni kuharisha kinyesi chenye damu, maumivu
ya tumbo na kuvimba tumbo"anaeleza Dkt. Nzalawahe.
Kama
nilivyoeleza awali Kichocho huwapata binadamu pamoja na wanyama
wafugwao kama Ng'ombe, Mbuzi na Kondoo kiitwacho (Bovine
Schistosomiasis) ambacho husababishwa na minyoo iitwayo Schistosoma bovis waishio
katika mishipa ya damu ya utumbo wa wanyama na kupelekea mnyama
kupunguza hamu ya kula, kuharisha damu, upungufu wa damu, mnyama kukonda na asipopata tiba mnyama hufa.
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa kichocho.
* Inatakuwa
kuacha kujisaidia haja kubwa au ndogo kwenye mabwawa, mito, maziwa na
mifereji ya maji. Kwa mtu mwenye kichocho (cha mkojo (Bilhazia)
anapokojoa mkojo hutoka na mayai ya kichocho, na kwa kichocho
cha tumbo, haja kubwa huwa na mayai ya kichocho ambayo huanguliwa mara
tu yanapogusana na maji na vijidudu vilivyo anguliwa huingia mwilini mwa
konokono na kuendelea kukua, baada ya wiki tano hutoka na kurudi kwenye
maji, ambako huogelea kutafuta mtu aliyepo ndani ya maji na huingia
kwenye mwili wa mtu kupitia kwenye ngozi.
* Inashauriwa
kuacha kuoga, kuchota, kufua nguo kwenye maji yaliyotuama kama vile
katika mabwawa, mito, maziwa na mifereji ambayo mingi inakuwa na konoko
wanaosambaza kichocho. Badala yake watu wawekewe maji ya bomba ambayo
huwekewa dawa za kuua vimelea vya maradhi.
* Inapendekezwa
kuondoa majani yaliyoota kwenye maji sehemu ambazo watu huenda kuchota
maji, kufua, na kuoga katika mabwawa, mito, maziwa, mifereji lengo likiwa ni kuharibu makazi ya konono.
* Mifereji
ya umwagiliaji isafishwe vizuri muda wote ili kupunguza uzalianaji wa
konono, na bora zaidi ni kuijenga mifereji kwa mawe na sementi, ili
kuharibu kabisa makazi ya konokono.
* Wakulima
wanaofanya kilimo cha umwagiliaji yafaa wavae mabuti na gloves
kujikinga na vijidudu vya kichocho kujipenyeza kwenye ngozi. Njia
nyingine ni kunyunyizia dawa za kuua konokono kwenye maji (ziwa, mto,
bwawa, mfereji), wenye konokono waenezao kichocho.
* Maji
ya kunywa yachemshwe na kuchujwa ili kuuwa vijidudu vya maradhi
mbalimbali ikiwemo wadudu wa kichocho. Unashauriwa pia kuchemsha maji ya
kuoga angalau kwa nyuzi joto 65 kwa muda wa dakika tano. Maji
yaliyohifadhiwa kwenye tanki kwa muda usiopungua masaa 48 ni salama kwa
ajili ya kuogea.
0 comments:
Post a Comment