Rais
wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam Mheshimiwa Truong Tan Sang ambaye
amewasili hapa nchini jana jioni tarehe 08 Machi, 2016 kwa ziara ya
kiserikali ya siku nne, amepokelewa rasmi na Mwenyeji wake Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini
Dar es salaam.
Katika
lango kuu lililopo Mashariki mwa Ikulu, Rais Truong Tan Sang amekagua
gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake na amepigiwa mizinga 21
iliyokwenda sambamba na nyimbo za mataifa yote mawili.
Pamoja
na mapokezi hayo, Marais hao wawili wamefanya mazungumzo ya faragha
ambayo yamehudhuriwa pia na makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan, na baadaye kufuatiwa na mazungumzo rasmi kati ya Rais Magufuli
na ujumbe wake na Rais Truong na Ujumbe wake.
Katika
Mazungumzo hayo, Rais Magufuli ameahidi kuuendeleza na kuuimarisha
zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Vietnam ambao
ulijengwa na waasisi wa mataifa haya mawili Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Hayati Ho Chi Minh, hata kabla ya Uhuru, huku
akitilia mkazo juu ya ushirikiano katika maendeleo ya kiuchumi.
Rais
Magufuli amemweleza Rais Truong Tan Sang kuwa katika miaka mitano
ijayo, Tanzania imedhamiria kujikita katika uanzishwaji wa viwanda
vingi, na hivyo ametaka mahusiano kati ya Tanzania na Vietnam
yajielekeze katika kuendeleza Kilimo na ufugaji na hivyo kuiwezesha nchi
kuwa na uhakika wa chakula na pia kupata ziada itakayouzwa nchi.
"Tunatambua
jinsi Vietnam ilivyopiga hatua kubwa katika uvuvi, uzalishaji wa kahawa
na uzalishaji wa mpunga. Uzalishaji katika maeneo hayo umeiwezesha kuwa
nchi inayoongoza duniani, na sisi Tanzania tunataka kujifunza kutoka
kwenu" Amesisitiza Rais Magufuli.
Kufuatia
hali hiyo, Rais Magufuli amemuomba Rais Truong Tan Sang, kuwa uhusiano
na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili ujikite katika kuendeleza kilimo
hususani kutumia zana bora za kilimo badala ya jembe la mkono, Kilimo
cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua, kuzingatia mbinu bora za
ugani, kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao na kupata masoko ya
mazao.
Kwa
upande wake Rais wa Vietnam Mheshimiwa Truong Tan Sang amempongeza Rais
Magufuli kwa kuchaguliwa kuiongoza awamu ya Tano na amemhakikishia kuwa
Vietnam itaendelea kushirikiana na Tanzania, huku ikitambua mchango
mkubwa uliotolewa na watu wa Tanzania walioiunga mkono juhudi za
kuiunganisha nchi hiyo na kuwa Jamhuri ya Kisoshalisti mwaka 1968.
Amesema
kwa kuzingatia mazingira bora ya Tanzania yenye amani na utulivu,
Vietnam imedhamiria kuwa Tanzania iwe kituo chake cha kuzifikia nchi
nyingine za Afrika Mashariki na sehemu nyingine za Afrika.
Rais
Truong Tan Sang ameomba mahusiano ya Tanzania na Vietnam, sasa
yajielekeze katika kuongeza Biashara, huku akieleza kuwa biashara ya
Dola za Marekani milioni takribani milioni 300 haitoshi, na hivyo
amependekeza wafanyabiashara wa Tanzania kuunganishwa na wenzao wa
Vietnam ili mauzo ya bidhaa kutoka pande zote mbili yaongezeke hadi
kufikia dola za Marekani bilioni 1 ifikapo mwaka 2020.
Ameongeza
kuwa Vietnam ipo tayari kutiliana saini mikataba mbalimbali ya
ushirikiano katika biashara, Viwanda na Kilimo, na ametoa mwaliko kwa
wakulima wa Tanzania kwenda kujifunza nchini Vietnam.
Mara
baada ya Mazungumzo hayo, Marais wote wawili wamezungumza na wananchi
kupitia vyombo vya habari ambapo wote wawili wamesisitiza kuwa, nchi zao
zipo tayari kukuza zaidi mahusiano na ushirikiano kwa faida ya wananchi
wake.
Gerson Msigwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam-09 Machi, 2016.
0 comments:
Post a Comment