NAMSHUKURU Mungu kwa kunikutanisha na wewe tena
msomaji wa safu hii ya Love Story. Huu ndiyo uwanja wetu wa kuweza kupeana mambo mbalimbali ambayo yanatu zunguka katika ulimwengu wa
uhusiano.
Ni ukweli usiopingika kwamba, mtu anapoanzisha uhusiano,
akadumu, siku zote hatarajii kama kuna siku penzi linaweza kuvunjika.
‘Anainjoi’ utamu wa mapenzi. Anapenda jinsi mwenzake anavyomjali na
kumuona wa thamani kuliko kitu kingine.
Akili na mawazo yake yote huwa yanakuwa kwa mpenzi wake. Kuna wakati
anapitiliza kupenda utafikiri kachanganyikiwa kumbe wapi, ni mapenzi tu
ndio yanampeleka puta. Anampenda mwenzake kiasi cha kuona kama wamekuwa
ndugu wa tumbo moja.
Ukaribu na mpenzi wake unamfanya ajisahau kabisa. Anafurahishwa na
ucheshi wake, utundu wake na kila kitu kinachagiza mapenzi. Dunia yote
anaiona kama ni yake na mpenzi wake. Wengine wote wasindikizaji tu. Hayo
ndiyo mapenzi!
Ukifika wakati penzi likayumba, likafa ghafla, mara nyinyi ambaye
hakuwa amejiandaa hupata maumivu makali ya moyo. Anapata maumivu kwa
sababu anakuwa hajajiandaa kisaikolojia. Akili yake iliamini watadumu
milele. Bahati mbaya mwenzake kwa wakati huo haumii sana kwa sababu yeye
alishajiandaa na pengine alikuwa hana lengo la kufika mbali na
mwenzake, alikuwa akimchezea tu.
Kwa yule ambaye hakujiandaa anateseka. Anakumbuka ukaribu aliokuwa
ameuweka kwa mwenzake. Namna ambavyo wamekuwa wakila, wakitoka ‘out’
pamoja na kufanya starehe mbalimbali za kusherehesha penzi ndivyo vitu
vinavyompa mawazo.
Anajiuliza kwamba ‘vurugu’ zote zile ndio zimefika ukingoni. Kwamba
kwa nini mwenzake hakumuweka wazi tangu mwanzoni kwamba hampendi ili
ajue moja?
Anawaza kumzoea kote mwenzake ndio kumefikia mwisho? Haamini. Hataki kukubaliana na matokeo. Anamuona mwenzake kama adui.
Hata kama mwenzake atamueleza kistaarabu. Kwamba kutokana na sababu
zilizo nje ya uwezo wake, haiwezekani kuendelea na safari. Bado inakuwa
ngumu kukubaliana na ukweli huo.
Kipindi hicho, ndicho cha kununiana. Aliyetendwa anaamua kumnunia mwenzake akiamini labda ndio dawa ya kumpunguzia machungu.
Hataki kabisa kumuona mwenzake. Anamnunia ileile. Anafika wakati hadi
marafiki wa aliyekuwa mpenzi wake nao anawanunia. Wote wanakuwa maadui,
anaamini wote lao moja. Kumbe pengine maskini ya Mungu, hawahusiki kwa
lolote.
Ndugu zangu, mapenzi siyo vita. Japo kweli penzi linapofikia kikomo
ambaye hakujiandaa siku zote huwa ni vigumu kukubaliana na matokeo
lakini tunapaswa kujifunza kufanya maamuzi ya busara.
Hakuna haja ya kununiana. Unavyoumia wewe, hata yeye anaweza kuumia pia. Kukuacha hujui amekuepusha na nini. Pengine haikupangwa muendelee na urafiki au kuwa wanandoa.
Ni vizuri ukamuweka mbali mtu mliyeachana lakini ikitokea mmekutana,
msalimiane.
Haikupunguzii kitu. Penzi linakuwa limeisha lakini ubinadamu
unabaki palepale.Kwa kipindi fulani, jaribu kukaa mbali na yule
mliyeachana. Haimaanishi umnunie, pata muda mwingi sana wa kufanya mambo
yako. Jishughulishe na vitu ambavyo vitakuondoa kabisa katika suala la
kuwaza mapenzi.
Usikurupuke kuanzisha uhusiano mpya kwani ni hatari sana kwa wakati
huo. Unaweza kuanzisha na mtu ambaye hana sifa nzuri na ukajikuta
unaambulia maumivu kwa mara nyingine.Baada ya muda fulani utazoea,
aliyekuacha mnaweza kuzungumza vizuri. Mkawa mnawasiliana kama kawaida
japo kwa wakati huo suala la mapenzi litakuwa halipo.
Mtakie kila la kheri katika safari yake kama kweli mtakuwa mmefikia
hatua ya kutorudi nyuma. Yawezekana mwenzako alifanya maamuzi yale kwa
kukurupuka, akajishusha na mkaendelea na safari kama kawaida.
Hakuna sababu ya kumnunia mtu ambaye mlikuwa kitu kimoja. Mlishirikiana na mambo mengi. Anakujua na wewe unamjua vizuri. Zidhibiti hasira. Hata kama alikosea kiasi gani, mfanye rafiki na maisha yaendelee.
0 comments:
Post a Comment