Wapigakura
wanne wa Jimbo la Bunda Mjini mkoani Mara, wamekamilisha taratibu za
kimahakama na kuwasilisha upya maombi ya kukata rufaa katika Mahakama ya
Rufaa ya Tanzania kutokana na maombi yao ya awali kutupiliwa mbali
Februari 24, mwaka huu.
Maombi
hayo yamewasilishwa na wapigakura Magambo Masato, Matwiga Matwiga,
Janes Ezekiel na Ascetic Malagila dhidi ya Mbunge wa Bunda Mjini, Ester
Bulaya, kuiomba mahakama hiyo kuwapa kibali cha kukata rufaa katika
mahakama hiyo.
Wapigakura
hao ambao wamekuwa wakimpigania aliyekuwa Waziri wa Chakula, Kilimo na
Ushirika na mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Bunda Mjini, Stephen Wasira,
waliwasilisha maombi ya kufungua shauri katika Mahakama ya Rufaa ya
Tanzania ili itoe ufafanuzi kuhusu haki ya mpigakura ya kuhoji matokeo
pamoja na vigezo vinavyotakiwa ili aweze kuhoji matokeo ya uchaguzi.
Maombi
yao ya awali yalitupiliwa mbali na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya
Mwanza, Sirilius Matupa kutokana na kuwasilishwa sura 141 ya sheria ya
rufaa na kueleza kuwa yalikuwa yamewasilishwa chini ya kifungu cha 15
(a) (b) badala ya kifungu 15 (c) ambacho ndiyo sahihi kwa ajili ya
maombi hayo na kuwaeleza wanaweza kurekebisha na kuyawasilisha upya.
Januari
25, mwaka huu Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mohamed Gwae,
aliitupilia mbali kesi namba moja ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Jimbo
la Bunda Mjini iliyofunguliwa na wapigakura hao dhidi ya Bulaya.
Wakati
huo huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Sumbawanga, Kakusulo Sambo
anayesikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi Jimbo la Nyamagana,
amekutana na mawakili wa pande zote na kuweka mikakati ya namna ya
kuiendesha.
Jaji
Sambo amekutana jana na mleta maombi (Ezekiel Wenje), mjibu maombi wa
kwanza (Stanslaus Mabula) pamoja na mawakili wanaowawakilisha kuweka
mikakati ya uendeshwaji wa kesi hiyo ikiwa ni pamoja na kubainisha
sehemu zinazobishaniwa.
Akizungumzia
hatua hiyo, Wakili Deya Outa anayemwakilisha Wenje, alisema katika
kikao hicho wamebainisha sehemu zinazobishaniwa na pande zote katika
kesi hiyo pamoja na mashahidi watakaotakiwa kufika mahakamani kutoa
ushahidi.
0 comments:
Post a Comment