Habari Mpya

Monday, May 02, 2016

Rais Magufuli Aagiza Askari wa Usalama Barabarani Aliyetukanwa na Mke wa Waziri Apandishwe Cheo

Rais John Magufuli ameagiza Koplo Deogratius Mbango kupandishwa cheo baada ya kumdhibiti mke wa waziri mmoja wa Serikali yake aliyepambana na askari huyo wa barabarani baada ya dereva wake kufanya kosa eneo la Namanga jijini Dar es Salaam.

Koplo Mbango alikumbana na tukio hilo baada ya dereva wa mke huyo wa waziri kusimama kwenye alama za kuruhusu watembea kwa mguu kuvuka barabara na alilazimika kupiga simu kituoni kupata maelekezo baada ya mama huyo kujitambulisha kuwa ni mke wa waziri.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha kazi cha makamanda wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa Serikali, na wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi, kilichofanyika mjini Dodoma, Rais Magufuli bila kumtaja jina alisema amemwonya waziri huyo na mkewe.

“Ebo! Yule trafiki anajua kazi, mpandishe cheo. Na huyo waziri na mke wake nimeshamwambia,” alisema Rais Magufuli, kwa mujibu wa taarifa ya habari ya TBC1.

Licha ya polisi na Rais Magufuli kutotaja jina la waziri huyo, mazungumzo kwa njia ya simu ambayo yamesambaa yanaonyesha mwanamke huyo aliyekamatwa akijitambulisha kwa jina la waziri mmoja mpya katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Majibizano ya polisi na mama huyo yanaonyesha kuwa dereva wake alikamatwa baada ya kusimama katikati ya mistari ya pundamilia, ambayo ni ishara ya kuvukia waendao kwa miguu.

Mazungumzo hayo yaliyorekodiwa yanaanza wakati Koplo Deogratius alipompigia simu kamanda wa trafiki wa Kinondoni, Mratibu Msaidizi wa Polisi, Awadh Haji na kumueleza tukio lililokuwa mbele yake.

Kadhalika Koplo Deogratius alimueleza RTO Haji kuwa wakati anataka kumuandikia faini, dereva huyo alitaka kuondoa gari na mama huyo akamtukana.

“Huyu mama akawa ananitukana… anasema yeye ni mke wa waziri. Nikamuambia hilo ni kosa la dereva, hivyo sitaruhusu aondoke bali nitampeleka kituoni. Wakati namuamuru dereva aende kituoni, akataka aondoke, nikamnyang’anya funguo ili nimpeleke kituoni,” alisema Koplo Deogratius.

“Ameniita mimi mshenzi, sina akili. Anasema yeye ni mke wa waziri gani?.. Anasema yeye sijui mke wa waziri (anamtaja jina).”

Baadaye Kamanda Haji anataka aongee na mama huyo ambaye mazungumzo yanaonyesha anakanusha kumtukana askari huyo, akisema alikuwa akimuomba amuelimishe dereva kwa kuwa kosa alilofanya ni dogo.

“Mimi sikumtukana, wala sikumwambia maneno hayo namshangaa sijui leo ameamkaje. Kitu nilichomuambia kwamba huyu kijana (dereva) alikuwa anakwenda moja kwa moja, mimi nilikuwa na vihela kidogo nilikuwa nataka kuchenji ili nimpe fundi,” alisema mke huyo wa waziri.

“Nikauliza kosa gani, akasema eti kosa lake ni kusimama kwenye zebra crossing. Nikamuambia sawa, hilo ni kosa la kuelimishwa, lakini sasa wewe unamuandikia kwa kosa kama hilo? Hilo ni kosa dogo, very minor la kuweza kumuandikia? Lakini kama unamuandikia andika.” 

Kupitia maongezi hayo, RTO Haji alisema kosa hilo ni kubwa na lina adhabu kali.

“Nikusaidie kitu kimoja, katika makosa mabaya sana mojawapo ni dereva kutoheshimu zebra crossing. Mahakama inapomkuta mtu na hatia ya kugonga kwenye zebra crossing, adhabu yake ni jela miezi sita. Haina hata faini, hiyo tunaita dangerous driving (uendeshaji wa hatari),” alisema Haji na kumtaka Koplo Deogratius kumuadhibu dereva kwa kosa lake.

Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Koplo Deogratius alikiri kupambana na mke huyo wa waziri, lakini hakutaka kuingia kwa undani akisema yeye si msemaji wa Jeshi la Polisi.

“Ni kweli nilimkamata huyo mama lakini, kwanza tuelewane. Mimi siyo msemaji wa polisi. Kama unataka kesho uje pale kituoni, umuone RTO. Kama akiruhusu mimi nitaeleza kila kitu,” alisema Deogratius akiwa maeneo ya Namanga. 

Naye Kamanda Haji alithibitisha tukio hilo, lakini akamuelekeza mwandishi kumuuliza kamanda wa polisi mkoani Kinondoni, Christopher Fuime.

Kamanda Fuime alisemai kuwa Rais Magufuli ameagiza koplo huyo apandishwe cheo kutokana na kusimamia sheria na kwamba agizo hilo linafanyiwa kazi.

“Mimi ndiyo natoka Dodoma kwenye hicho kikao cha Rais na maofisa wa polisi. Hilo ni agizo, sasa unataka tulipinge? Hayo ni mambo ya utawala, wataangalia wenyewe kama apewe cheo gani. Kwa sasa yeye ni Koplo, kwa hiyo watajua wenyewe wampe nini. Afande IGP ndiyo anajua,” alisema Fuime.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Item Reviewed: Rais Magufuli Aagiza Askari wa Usalama Barabarani Aliyetukanwa na Mke wa Waziri Apandishwe Cheo Description: Rating: 5 Reviewed By: mcjohnminja.blogspot.com
Scroll to Top