Habari Mpya

Tuesday, June 07, 2016

PASTOR NICK SHABOKA ATOA WARAKA MZITO KWA WATUMISHI WA MUNGU,USOME HAPA.

HUU NI WARAKA WA SHABOKA KWA WATUMISHI WA MUNGU.
Karibuni kila msikiti unakisima cha maji ya chumvi ambayo kinagawa bure au kuuza kwa jamii zetu za kitanzania, na wanawake wengi wa kikristo na washirika wa makanisa yetu wanaenda kuchota maji hapo. Na hao maustadhi (vijana wa kiislam) waliopewa kusimamia mradi huo ni wakali hawaruhusu mwanamke yeyote kuchota maji bila kufunika kichwa (kuvaaa kilemba) ili kufuatisha sheria ya dini ya kiislamu na wanawake wetu wanafuatisha kwani wanahitaji huduma ya maji. 


Sisi tumebaki kukazana kujenga makanisa makubwa na mazuri na kununua maspika makubwa yanayosumbua majirani zetu kwa kero ya sauti za nyimbo za kwaya na waimbaji wetu zisizo na tija kwa jamii, lakini huduma za jamii kwa makanisa ya kiroho tumejiweka mbali nazo sana. Tunajua kugawa bahasha za mbegu na kufundisha watu aina tisa za sadaka lakini hakuna kitu tofuti na maombezi ambacho kinaweza kuwaleta wasio wa wakristo kushiriki nasi. Ni wakati wa kuamka.
 

Wakatoliki na walutheri wamejitahidi kugusa jamii katika eneo la elimu na miradi ya fedha (Vicoba, Saccos, na mabenki) pamoja na Afya kwa kujenga Zahanati na Mahospitali, walokole tumekalia kuhubiri tu ubatizo wa maji mengi nakukosoa ibada zao za sanamu, wakati kwa jamii hatuna msaada wa kimwili.
 

Cha ajabu hata makanisa ya kiroho yenye washirika wengi yameshindwa kuendeasha hata vituo vya watoto yatima! Mungu anashangaa. Radio zetu zimejaa mahubiri tu na nyimbo na kupondana sisi kwa sisi, lakini vipindi vya Afya, mahusiano, elimu na biashara ni vichache au hakuna. Tunapowaachia wengine kutufundishia washirika wetu jua wazi kuwa wanapanda na roho zao ndani ya watu wetu.
 

Runinga zetu zimekuwa mali ya huduma, kazi ni kuchangishia pesa tu, hazileti umoja wa kanisa bali zina vipindi zaidi ya 10 vyenye kutukuza na kumsifia founder wa huduma. Ndio maana uislamu na imani zingine unakua kwa kasi wakati Ukristo ukizidi kuporomoka na kupoteza umaarufu.
 

Tukumbuke Yesu alilisha watu zaidi ya elfu tano katika Yohana 6, na akaagiza tujitie nira yake na kujifunza kwake Mathayo 11:29, hii inamaana tufanye kama yeye alivyofanya, maisha yake na huduma yake ni muongozo wetu, katiba, kanuni na msingi wa huduma zetu. Kama alilisha mikate watu zaidi ya elfu tano kwa muujiza, maana yake mimi na wewe tunapaswa kuwa na shamba la mahindi au mpunga ambalo ni mradi wa kanisa unaoweza kulisha watu millioni moja katika jamii zetu. 

Huko ndio kujifunza kwa Yesu kwa kufanya aliyoyafanya. Kama aliponya jamii kubwa ya wagonjwa nasi pia tunapaswa kuwa na Hospitali zenye idara mbali mbali kama X-ray, Orthoepadic, Uzazi, watoto, Upasuaji, ili wale wasioweza kuja kwenye maombi wakamatwe kwa njia ya tiba huku wakitazama mikanda ya mahubiri katika ward zao na kusikiliza nyimbo za injili wanapokuwa mazingira ya hospitali.

Nisiseme mengi, Tanzania, Afrika tufufuke katika wafu, tuachane na usingizi wa mapokeo na mashindano. Kuna mambo makubwa ya kufanya na njia rahisi sana za kuhubiri kukiko kukazana kuandaa mikutano mikubwa ya injili inayobagua aina ya watu wakutusikiliza na kufikiwa.


Hiyo gharama ya mkutano wako wa injili ulioandaa kwa milioni sitini, ungemlipa mtaalamu wa macho na kununua aina mbalimbali za miwani kwa hiyo pesa na kupeleka wiki au siku tatu za clinic ya kupima macho na miwani kanisani kwako na ukapata muda wa kushare injili na hao watakaokuja ingekuwa na mguso mkubwa na kuacha alama kwa jamii inayokuzunguka na kuongeza idadi ya waumini kwa kanisa lako.
Nisiseme mengi. Mungu atusaidie.



Kwa hisani ya GospelMedia
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Item Reviewed: PASTOR NICK SHABOKA ATOA WARAKA MZITO KWA WATUMISHI WA MUNGU,USOME HAPA. Description: Rating: 5 Reviewed By: mcjohnminja.blogspot.com
Scroll to Top