Habari Mpya

Tuesday, June 07, 2016

Kanisa Katoliki jimbo la Dar es Salaam Kutoa Zawadi Kwa Ndoa Kongwe

NDOA ni taasisi, na jamii inaamini kwamba, kuwa kwenye ndoa ni baraka hivyo inastahili kuthaminiwa. Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam linataka kuonesha mfano katika hilo kwa kuamua kuwatunuku tuzo wanandoa wakongwe zaidi katika jimbo hilo.Wanandoa wamepewa tuzo ikiwa ni moja ya kumbukumbu ya maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu. Wanandoa hao walitarajiwa kutunukiwa tuzo maalumu jana katika ukumbi wa Maranta, Msimbazi Centre jijini Dar es Salaam.

Askofu Msaidizi wa jimbo hilo, Eusebius Nzigilwa, alitarajiwa kukabidhi tuzo kwa wanafamilia watatu wanaoaminika kuwa ndoa zao ni kongwe kuliko nyingine. 

Askofu Nzigilwa pia alitarajiwa kutoa baraka kwa wanandoa. Mmoja wa waratibu tuzo hizo, Nolascus Mpota alisema, tukio hilo lilitarajiwa kuandaliwa na familia ya wanamaridhiano na kusimamiwa na Idara ya Kichungaji na Utume wa Familia ya Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

“Tumepata uthibitisho wa ndoa yenye umri wa miaka 61, kutoka Parokia ya Chang’ombe na ile ya miaka 57 kutoka Parokia ya Oysterbay. Hata hivyo, tunasubiri uthibitisho wa ndoa yenye umri wa miaka 67 ambapo kwa sasa wanandoa hawa wakongwe wako Mahenge, walikokwenda wiki mbili tu zilizopita wakitokea Segerea walikokuwa wakiishi, na tunaamini huenda ndio ikawa ndoa kongwe kuliko nyingine zote jijini Dar es Salaam,” anasema Mpota.

Anasema, lengo la tuzo hizo ni kuwakumbusha wanandoa kuhusu umuhimu wa kutunza na kuheshimu maisha ya ndoa na kutambua baraka na huruma ya Mungu inavyowasaidia wanandoa na wanafamilia katika maisha yao.

“Ni siku ya kutoka “out” na mwenzako wa ndoa, kula na kunywa na wanandoa wengine, hivyo tunawakaribisha wanandoa…” alisema Mpota. Watanzania wakongwe kwenye ndoa wamepewa tuzo hizo wakati kukiwa na kumbukumbu ya shehere ya miaka 89 ya ndoa iliyofanyika mwaka 2014 nchini Uingereza.

Wakati huo iliaminika kwamba, Karam Chand na Kartari Chand walikuwa wanandoa walioishi kwenye taasisi hiyo kwa miaka mingi zaidi. Wakati wanafurahia miaka 89 ya ndoa nyumbani kwao Bradford, West Yorkshire, Karam alikuwa anatimiza umri wa miaka 109 na mkewe miaka 102.

Hadi wakati huo, wanandoa hao walikuwa na vizazi vinne wakiwemo watoto wao wanane, wajukuu 27, na vitukuu 23. Karam na Kartari walifunga ndoa Desemba mwaka 1925. Walikutana India wakiwa vijana na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi.

Karam alizaliwa mwaka 1905 kijijini kwenye mkoa wa Punjab uliopo kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Alifunga ndoa na Kartari wakati mwanamume huyo akiwa na umri wa miaka 20.Wazazi wa Karam walikuwa wakulima na ilibidi aoe akiwa na umri huo ili kutunza tamaduni zao. Kartar alizaliwa mwaka 1912 kwenye eneo hilo hilo, na alifunga ndoa akiwa na umri wa miaka 13.

Karam na mkewe walihamia Uingereza mwaka 1965. Kwa sababu ya uzee, wakati wa sherehe ya kutimiza miaka 109 mwanaume huyo alikuwa akitembea kwa taabu. Karam anasema ameweza kuishi maisha marefu akiwa na afya hajawahi kuacha kufurahia maisha yake. “Kula, kunywa unachotaka lakini kwa kiasi,” anasema mzee huyo.

Mtoto wa wanandoa hao, Paul alisema alifurahi kuwasaidia wazazi wake kusherehekea pamoja siku yao ya kuzaliwa sanjari na kutumiza miaka 89 ya ndoa. “Imekuwa siku maalumu kwa familia yangu na sisi wote kuweza kujumuika kama hivi… ndugu ‘wamepaa’ kuja India kuwa nasi…watu wametiwa sana na wazazi wangu,” anasema Paul.

“Kila mara wananiuliza, unakula nini, unawalisha nini na wanawezaje kubaki na afya njema?” anasema Paul. “Ninawaambia kama ningejua hilo na mimi ningekuwa kama wao…Kila mtu wanawezaje kuwa na afya na jibu langu ni kwamba, kwa miaka 20 iliyopita tumewapa maisha yasiyo na msongo wa mawazo,” anasema. Imeandikwa na Gloria Tesha na Basil Msongo
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Item Reviewed: Kanisa Katoliki jimbo la Dar es Salaam Kutoa Zawadi Kwa Ndoa Kongwe Description: Rating: 5 Reviewed By: mcjohnminja.blogspot.com
Scroll to Top