Wakati Rais John Magufuli akitarajia kuwasili Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) leo, wanafunzi walioandamana wakishinikiza malipo yao ya
fedha za kujikimu juzi, huenda wakakumbwa na hatua za kinidhamu.
Wanafunzi
hao huenda wakaadhibiwa kwa kosa la kukikuka sheria ndogo ya chuo kwa
kuandaa mkusanyiko pasipo kibali cha menejimenti.
Naibu Makamu
Mkuu wa Chuo (Taaluma), Florens Luoga alisema jana kuwa, mamlaka za
nidhamu chuoni hapo zinaendelea na uchunguzi kubaini nani aliyehusika
katika tukio hilo.
“Taratibu na sheria ndogo za chuo haziruhusu
mtu kuandaa mkusanyiko ambao haujaidhinishwa na menejimenti. Taratibu
hizo lazima ziheshimiwe ili ziendelee kuwa imara. Hivyo tunasubiri
ripoti ya waliohusika,” alisema Luoga.
Juzi, wakati wa
maandamano ya wanafunzi hao walikuwa wakipaza sauti iliyotolewa na Rais
Magufuli wakati wa kampeni za kuwania wadhifa huo akisema:
“Serikali
yangu haitarajii kuona mwanafunzi akifukuzwa chuo kwa kosa la kugoma
kisa mkopo, bali ikitokea mgomo, watawajibisha maofisa wa Bodi ya Mikopo
kwa kuchelewesha fedha.”
Taarifa zilizopatikana jana zilieleza kuwa fedha za wanafunzi hao zimeshawekwa kwenye akaunti zao, juzi jioni.
Rais
wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Erasmi Leon alisema licha ya
wanafunzi hao kukiuka utaratibu, haoni sababu za kuwachukulia hatua
kwani hawakusababisha madhara wala uharibifu wowote.
“Endapo
kamati ya nidhamu itaamua kufanya hivyo ni vyema wakafanya suala hilo
kimantiki na kibinadamu na endapo usimamizi wa sheria ukifuata zaidi
unaweza ukasababisha kuibuka kwa mambo mengine tofauti,” alisema Leon.
Alisema
wanaendelea kuwasihi wanafunzi kuhakikisha suala hilo halijitokezi tena
kwani linaitia doa Serikali yake, uongozi wa chuo na Taifa kwa jumla.
Wanafunzi
hao waligoma kuanzia Jumatatu usiku na mgomo wao kuisha juzi, baada ya
kupewa fedha zao ambazo zilichelewa kwa madai ya uhakiki wanafunzi hewa
unaondelea.
0 comments:
Post a Comment