Habari Mpya

Tuesday, July 26, 2016

Nguvu ya Roho Mtakatifu-Mwl C.Mwakasege

Je! Umewahi kujiuliza kwa nini wakati mwingine nguvu za Mungu zinakushukia kwa uwingi halafu baada ya muda zinapungua au zinaondoka – unabaki hali kama vile hujawahi kushukiwa hata siku moja? Inawezakana umewahi kujiuliza swali hili na inawezekana hujawahi kujiuliza. Na pia inawezekana hali hii tunayoiuliza hapa juu haijawahi kukutokea. Kumbuka kuwa nguvu za Mungu zinaweza kupungua ndani yako – kwa sababu mbalimbali – ambazo ni pamoja na kutozitumia kwa kiwango kilichokusudiwa. Unakumbuka Yesu alipoulilia mji wa Yerusalemu? Alisema; “Laiti ungalijua, hata wewe, katika siku hii, yapasayo amani!” (Luka 19:42).

Alichokuwa anataka wajue ni kwamba ndani yake kulikuwa na nguvu au upako wa Roho Mtakatifu uletao amani. Lakini tunaona wazi ya kuwa Yerusalemu hawakutumia upako huu na amani ya Mungu ikaondoka pia. Tatizo la Yerusalemu lilikuwa ni kwa sababu hakutambua majira ya ‘kujiliwa’ kwake. Kwa lugha nyingine Yerusalemu ‘ulijiliwa’ au ulitembelewa na nguvu za Mungu ziletazo amani – lakini hawakutambua! Na kwa sababu hawakutambua hilo, kwa hiyo hata nguvu za Mungu hawakuzitambua wala kuzitumia. – Kilichotokea ni kwamba nguvu hizo (1Wakorintho 1:18,24) ziliondoka wasiweze kuzitumia.

Tunaona pia katika Yohana 1:11 ya kuwa “ Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea.” Yesu anaweza kuja kwako. Nguvu zake (ambazo ndizo nguvu za Roho Mtakatifu) zinaweza kuja kwako – usipozipokea itakuwa vigumu kuzitumia kwa kiwango kinachotakiwa. Maana katika mstari unaofuata wa 12, Yohana anaendelea kusema hivi: “ Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika …..” Ili uweze kuzipokea na kuzitumia nguvu za Mungu ipasavyo ni vizuri ujue Mungu amezituma nguvu zake kwetu kwa ajili ya nini. Zipo sababu nyingi katika biblia, lakini sisi tunataka tukupe angalau chache wakati huu ili ziwe changamoto kwako.

Sababu ya Kwanza: TUWE MASHAHIDI WAKE
Ili tuonekane na kujulikana ya kuwa sisi tu wanafunzi wa Yesu – tunachohitajika kufanya ni kupendana (Yohana 13:35). Huu ni upendo ambao watu wasiomjua huyu Mungu wetu  wanatakiwa wauone kwetu. Wakiona tunavyopendana, basi watajua ya kuwa sisi tu wanafunzi wa Yesu. Unapofanya sala ya toba na kumkaribisha Yesu katika maisha yako – unaokoka. Unaweza ukawa umeokoka lakini usiwe ‘mwanafunzi’ wa Kristo – kwa tafsiri ya Yesu juu ya nani ni mwanafunzi wake. Ikiwa umeokoka na huonyeshi upendo wa Kristo kwa waliookoka wenzako unapoteza hadhi ya kuwa mwanafunzi wa Kristo.

Inapofika hali ya kuwa ‘shahidi’ inabidi upokee nguvu za Roho Mtakatifu. Yesu alisema katika kitabu cha Matendo ya Mitume 1:8 ya kuwa: “ Lakini mtapokea nguvu,; akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi” Kazi ya shahidi ni kusimama upande wa anayeshitaki au anayeshitakiwa kumtetea huyo ambaye ameamua kuwa shahidi upande wake – akisema na kwa kuonyesha vithibitisho ili kusisitiza kuwa anachokitetea ndicho sahihi.

Katika mazingira ya Bwana Yesu, sisi tunakuwa mashahidi kwa kusema na kuonyesha au kuthibisha kwa vitendo ya kuwa yote ambayo Yesu Kristo amesema na yamefanyika juu yake ndivyo yalivyo, na ndiyo kweli inayotakiwa kufuatwa na kila anayemtafuta Mungu wa kweli. Nguvu za Roho Mtakatifu zinatufanya tuweze kusimama katika nafasi ya kuwa mashahidi wa Kristo.
hs as teacher 9

Sababu ya Pili: Kushinda Dhambi

Ndiyo! Kushinda dhambi. Unaweza kuishinda dhambi. Katika Mwanzo 4:7 tunaambiwa inatupasa au ni lazima tuishinde dhambi. Mungu hawezi kusema tuishinde dhambi kama hakuna mbinu ya sisi kuishinda dhambi. Pia, katika Warumi tunaambiwa ya kuwa dhambi haitatutawala. Lakini ni lazima tujue ya kuwa hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kuishinda dhambi kwa nguvu zake mwenyewe. Kila mtu lazima ajue kuzitumainia nguvu za Mungu tunazozipata katika Roho Mtakatifu kwa sababu ya Kristo kufa msalabani kwa ajili yetu.

Ndiyo maana imeandikwa hivi katika 1 Wakorintho 1:18,23,24: “ Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookokolewa ni nguvu ya Mungu …… sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu.” Hiki ndicho kinachotokea unapookoka; Kristo anaingia ndani yako kwa uwezo wa Roho Mtakatifu- anakuwa nguvu ya Mungu inayokuwezesha kushinda dhambi. Kwa hiyo kama iko dhambi inayokusumbua – tubu, halafu omba Mungu akuongezee nguvu za Roho wake ili upate kushinda dhambi.

Sababu ya Tatu: Kuwa Tajiri
Jambo mojawapo lililotokea kwa mwanadamu dhambi ilipoingia ni kuishi maisha ya umaskini na kupungukiwa. Dhambi pia iliweka matabaka ya matajiri na maskini. Toka mwanzo na hata sasa na siku zote Mungu hapendi watu wake wawe maskini (kwa jinsi ya mwili) Katika 2 Wakorintho 8:9 tunasoma ya kuwa: “ Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake” Kwa hiyo ni mapenzi ya Mungu tuwe matajiri.

Njia ambayo Mungu anatumia kutuwezesha tuwe matajiri ni kwa kutupa nguvu zake. Kwa maana imeandikwa katika kitabu cha Kumbukumbu ya Torati 8:18 ya kuwa: “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri, ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo” Tunasoma hapa ya kuwa tunaweza kuomba tupate msaada wa nguvu za Mungu ili tupate utajiri halali ndani ya Kristo.

Sababu ya Nne: Kushinda hila za shetani
Tunasoma katika kitabu cha Waefeso 6:10,11 ya kuwa: “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 

Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani” Haitoshi kupokea nguvu za Roho Mtakatifu bila kuwa hodari katika kuzitumia ili upate “kuweza kuzipinga hila za shetani” Ili uwe hodari katika mchezo fulani lazima ufanye mazoezi ya kutosha ili kujifunza mbinu za kukusaidia kushinda upinzani katika mashindano. Pia, katika mambo ya rohoni ni vivyo hivyo.

Ili uwe hodari katika uweza wa nguvu za Mungu – haitoshi tu kuzipokea kwa kujazwa Roho Mtakatifu. Bali ni muhimu kufanya ‘mazoezi’ sawa na neno la Mungu ili uwe hodari. Hii ndiyo maana unaweza ukajawa nguvu za Mungu na bado shetani akakushinda na hila zake. Kwa nini? Kwa sababu hujazwa hodari katika kuzitumia. 

Hii ni sawa na mtu kuwa na silaha yenye nguvu vitani lakini kwa sababu hajui kuitumia ipasavyo anajikuta ameshindwa vita! Nguvu za Roho Mtakatifu zipo pia kwa ajili ya kutusaidia kumshinda shetani na hila zake dhidi ya maisha yetu. Lakini ni muhimu tujue kuzitumia sawa na neno la Mungu – tuwe hodari katika uweza wa nguvu zake. La sivyo tutakuwa tunashindwa na shetani wakati tunazo nguvu za kumshinda ndani yetu.
hs as teacher 9
Sababu ya Tano: Kudumu katika maombi
Kila mtu aliyeokoka ndani yake anahamu ya kufanya maombi – kuzungumza na Mungu. Lakini karibu kila mtu anajua ya kuwa kila akiomba anatamani angeweza kuomba vizuri zaidi, kuliko anavyoomba wakati huo.

Jambo hili la kuwa na upungufu katika maombi lisikushangaze. Biblia inatuambia; “…. Hatujui kuomba jinsi itupasavyo ….” (Warumi 8:26). Kazi ya Roho Mtakatifu ni kutusaidia udhaifu huu tulionao wa kuomba – ili kwa nguvu zake tuweze kuomba utupasavyo, na pia tuweze kuwaombea “watakatifu kama apendavyo Mungu” (Warumi 8:27). uzuri wa maombi si tu kwamba ni sababu ya Mungu kutupa Roho wake ili kwa msaada wa nguvu zake tuweze kuomba itupasavyo; bali maombi pia ni njia au mlango wa nguvu za Mungu kuongezeka katika maisha yetu. Ndiyo maana mara nyingi ukikaa katika maombi muda mrefu zaidi – nguvu za Mungu zinaongezeka.

Lengo la nguvu hizi kuongezeka ni ili uendelee kuomba kama impendezavyo Mungu hadi upate unachoomba. Kwa mfano, kama nguvu za Mungu ni kidogo ndani yako – hasa wakati umo taabuni au katika majaribu – ni rahisi sana ‘kuzimia’ au kukata tamaa. Imeandikwa hivi: “Ukizimia siku ya taabu, nguvu zako ni chache” (Mithali 24:10) “Bali vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka, bali waowamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia” (Isaya 40:30,31) Nguvu za Mungu ndani yako zitakusaidia usizimie wala usichoke wala usikate tamaa iwe ni wakati wa raha au wakati wa taabu. Ukiona unachoka au unakata tamaa maana yake una nguvu kidogo au zimepungua – kwa hiyo omba Mungu akuongezee nguvu zake ili usichoke wala kuzimia wala kukata tamaa.

Sababu ya Sita: Kuondoa woga
Mtume Paulo aliwahi kumwandikia Timotheo maneno muhimu sana ambayo yanasema na watu wengi hata sasa aliposema; “ Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi” (2 Timotheo 1:7) Timotheo asingeandikiwa maneno haya kama hakuwa mwoga! Inaonyesha alikuwa mwoga kuichochea ‘karama ya Mungu’ iliyokuwa ndani yake! (2 Timotheo 1:6) Kama alikuwa mwoga basi hali hii ilifanya utumishi wake ulegee.

Hii inawezekana ilitokea kwa sababu aliona na kushuhudia mateso aliyopata Mtume Paulo alipochochea karama ya Mungu iliyokuwa ndani yake. Kwa kuogopa kuteswa na yeye kama Mtume Paulo, aliamua kuacha kuchochea karama ya Mungu iliyokuwa ndani yake. Ndiyo maana Mtume Paulo  alimhimiza aichochee hiyo karama “….maana Mungu hakutupa roho ya woga bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi” Kama unasikia woga wa kumtumikia Mungu kwa sababu moja au nyingine hauko peke yako.

Dawa yake ni nguvu za Mungu ziongezeke ndani yake- na woga huo utaondoka! Timotheo alibanwa na woga. Lakini pia Yoshua alipokuwa anakabidhiwa wajibu wa kuongoza wana wa Israeli baada ya Musa kufa – alishikwa na woga! La sivyo Mungu asingemwambia awe na moyo wa ushujaa mara tatu! (Yoshua 1:6,7,9).

Yeremia naye alipokuwa anapewa wajibu wa kumtumikia Mungu akiwa bado mtoto – aliingiwa na woga! Lakini Mungu akamwambia – “Usiogope” (Yeremia 1:4-10). 

Kwa hiyo kama unasikia woga katika kumtumikia Mungu – omba ili Mungu akupe nguvu zake zaidi ili ziondoe woga. Jambo hili liliwahi kumtokea Mtume Petro. Pamoja na kwamba alimpenda Yesu sana na kuahidi kuwa naye kila mahali – bado woga ulimwingia alipoulizwa kama alimjua Yesu wakati Yesu amekamatwa. 

Lakini  baada ya kujazwa nguvu za Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste hatuoni tena woga ukijitokeza ndani yake – bali tunaona ujasiri mwingi.

Na Mwl Christopher Mwakasege

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 comments:

Item Reviewed: Nguvu ya Roho Mtakatifu-Mwl C.Mwakasege Description: Rating: 5 Reviewed By: mcjohnminja.blogspot.com
Scroll to Top